Mizizi ya mihogo haina virutubisho muhimu vya chuma na zinki kwa viwango vya kutosha vinavyohitajika vya kila siku, hasa kwa wanawake na watoto. Aina ya mihogo iliyo na viwango vya juu vya chuma na zinki vingeweza kutoa mchango mkubwa wa lishe na afya kwa familia katika Afrika.

 

Mahitaji: Mihogo yenye lishe zaidi

 

Anemia (ukosefu wa damu) unaotokana na upungufu wa chuma mwilini huathiri mfumo wa kinga, kudumaza kukua na kuharibu maendeleo ya utambuzi kwa watoto, wakati upungufu wa zinki husababisha hatari ya vifo kutokana na kuharisha, kudumaa na kutokua kwa utambuzi kiakili.

Katika Nigeria peke yake, asilimia 75 ya watoto wa shule za awali na asilimia 67 ya wanawake wajawazito wana upungufu wa damu (anemia) na katika Afrika kusini mwa jangwa la Sahara inakadiriwa kuwa asilimia 24 ya idadi ya watu wako katika hatari kutokana na upungufu wa zinki uliosababishwa na ukosefu wa kula chakula cha kutosha.

Mizizi ya mihogo ni chanzo bora sana cha wanga wa bei nafuu wakati wote, lakini ina kiasi kidogo sana cha chuma na zinki zinazohitajika katika chakula cha afya njema. Msingi wa chanzo cha chuma na zinki kwa watu maskini wa mjini na vijijini wasio na raslimali unapatikana kwa kula vyakula vya mimea, hasa aina ya maharage, mboga za majani na nafaka nzima (zisizokobolewa). Hata hivyo, upatikanaji wa kiasi cha chakula kinachohitajika mara nyingi ni kwa msimu tu na hakuna uhakika wa ubora wake.

 

Kazi yetu: kukuza aina za mihogo zenye viwango vya juu vya chuma na zinki.

 

Watafiti hawajaweza kuongeza kiasi cha chuma na zinki kwenye uhifadhi wa mizizi ya mihogo kwa kupitia njia za desturi (kawaida) za uzalishaji wa aina za mihogo kuchanganya na ile jeni yenye uzao wa kufanana. (breeding lines) Uhandisi wa ugeuzaji jeni hutumiwa kuingiza jeni mbali kutoka kwenye mmea mwingine, ‘arabadopsis’ ambayo inafanya kazi ya kuinua kiasi cha chuma na zinki kwenye mizizi ya mihogo.

Tumefanikiwa katika kuendeleza na kupima mimea ya mihogo ambayo inakusanya chuma na zinki zaidi ya mara 10 ikilinganishwa na zingine.

Majaribio ya shambani yalionyesha kwamba mizizi ya mihogo ina uwezo wa kutoa makadirio vya asilimia 40-70 ya wastani wa mahitaji ya madini haya kwa kina mama na watoto wa hali ngumu wanaoweza kudhurika. Mizizi ya mihogo yenye lishe bora inaweza kuhifadhi viwango vya juu vya chuma na zinki hata baada ya kuimenya, kuichemsha na kuitengeneza kwa njia zozote zinazotumiwa kuandaa vyakula vya kawaida vya Afrika magharibi, kama ‘gari na fufu’.

Uzalishaji pia hutumiwa kuingiza hizi sifa bainishi kwenye aina za mihogo ya mazao mengi ili kukidhi mahitaji ya wakulima na walaji. Aina za mihogo ambazo zinapendelewa na wakulima na watumiaji nchini Nigeria na nchi zingine za magharibi mwa Afrika zitakuwa za kwanza kwenye mpango wa kuimarisha lishe wa ‘VIRCA PLUS’.